MALEZI YA WATOTO NA FAMILIA – 1

0 89

Neno la Utangulizi

Malezi ya watoto na vipi familia zetu zinatakiwa kujengwa kwa mujibu wa maadili yetu ya kiislamu ni jambo la muhimu sana kuzungumziwa katika kila fursa. Katika Makala hii tutajitahidi kueleza kwa mtindo wa kipekee na hivyo tunaamini kuwa Makala hizi zitakuwa na mchango mkubwa katika kutoa mtazamo mzuri juu ya swala la familia na malezi ya watoto kwa ujumla.


Tunamuomba Allah (s.w) atuwezeshe katika kazi hii na pia aifanye kuwa ni kazi yenye faida kwa wasomaji wetu wa lugha ya Kiswahili kote ulimwenguni.

Ufahamu Wetu wa Tabia Njema

Tujiulize juu ya maana ya maadili

Kwa hakika ni lazima kwanza kuafikiana na wasomaji wetu watukufu baadhi ya masuala kwa sababu tunaamini kuwa kufaidika na Makala hii hakutawezekana bila ya kuafikiana katika masuala ya msingi. Je, inawezekana– wakati wa kujadili maudhui yanayohusu malezi katika familia– kuafikiana kuhusu maana ya maadili pamoja na wasiokereketwa na wingi wa mabaya katika nchi yetu, mji wetu, kijiji chetu na nyumba yetu?


Na ni lipi tunaweza kusema ikiwa tumeridhia hali yetu pamoja na yote hayo, na tutasema nini ikiwa mabaya yaliyotuzunguka hayajatuathiri? Na je, inawezekana kuwa na taswira ya faida inayotarajiwa ya kusomeshana masuala ya kimaadili nyoyo zetu zisipotetemeka na kuchukia mmomonyoko wa kimaadili tunaouona kwa watoto wetu, wajukuu zetu, watoto wa ndugu zetu, ambao sisi ni wajomba zao, baba zao na majirani zao?


Jamii zilizodumu zilikuwa zikiheshimu maadili mema.

Katika historia hakuna jamii iliyobakia baada ya kudhihiri uharibifu ndani yake, na wala sijui kama kuna jamii ambayo imeenda kinyume katika hili, lakini hapana shaka kuwa umma zilizolinda uwepo wake kwa muda mrefu bila ya kutengwa na historia zilikuwa zikiheshimu maadili mema.

Sababu za Kuporomoka kwa Mataifa

Maadili Mabaya Ni Kama Saratani

Tukitazama staarabu mbalimbali zilizopita tutakuta kuwa sehemu kubwa ya kuporomoka kwa staarabu hizi ni kuharibika kwa maadili. Na wakati mwingine hatuhisi ubaya wa maadili mabaya yanapokuwa yakiingia kidogokidogo kwenye tamaduni ya jamii, na tunapohisi muda unakuwa umeshapita, mfano wa saratani.


Saratani ilivyokuwa hatuwezi kujuwa uwepo wake ila baada ya kufika katika sehemu muhimu katika mwili. Na baada ya kifo kukaribia na kuanza safari ya akhera, basi ni hivyohivyo maadili mabaya yanavyofanya kwa taifa lolote lile.


Ndiyo, kama ambavyo saratani inafanya katika mwili wa mwanadamu basi pia maadili mabaya yanafanya hivyo hivyo kwa maisha ya umma zote. Viongozi wa nchi, wasimamizi, walezi wa familia na umma kwa ujumla wakighafilika na mmomonyoko kama huu wa kimaadili, basi umma wote utaporomoka kwa kishindo. Na pengine baadhi wasizinduke kutokana na kughafilika, hata kama nguzo za umma zote zitaporomoka, na huenda wengine wakaona ni kawaida kama vitongoji vilivyopo maeneo yaliyoharibika kwa kisingizio kuwa hayo nayo ni maisha.

Baadhi Ya Sababu Za Kuporomoka
Ndiyo, tukitazama kwa ujumla katika sababu za msingi za kuporomoka kwa umma tofauti tutaona zinarejea kwenye sababu zifuatazo:


Ni vijana kukosa umakini, kukosa kwao heshima na kupendelea kukuza hisia za kinyama (kama vile kula, kunywa, kulala, na mahusiano ya kimwili) kwa madai ya kuwa wapo huru. Pia kuzama katika matamanio, jamii kuipenda sana dunia na kuisahau akhera, kuwa mbali na Allah, kuipuuza Qur’an, na nyoyo kukosa hofu (ya Allah). Aidha kila kitu kuelekezwa katika mambo ya kidunia (kufanya kila kitu kwa lengo la hela(pesa), cheo, kujifaharisha n.k, na si kwa ajili kusaidia watu na kutafuta radhi za Allah (s.w.t)).


Miongoni mwa sababu nyingi kati ya hizi ndizo sababu za kuporomoka kwa nchi nyingi ikiwemo Dola la Ottoman, na wakati ambapo walikuwa wanataka kumalizana na matatizo yaliyoletwa na upungufu wa mambo ya kiroho, tahamaki wanajisaidia kwa mambo ya kidunia ambayo yanazidisha ukali wake, na wakaingia katika mahala palipoharibika kabisa, ingawa tatizo linatokana na mataifa kupoteza hali yake ya kiroho na kuwa mbali na Qur’an, misingi ya Uislamu na kumsahau Mola wao aliyetukuka.


Mwili na Roho Vipewe Haki Sawa

Chanzo cha kupotea kinaeleweka na kipo wazi; kwani kila kitu kinatokana na kuzama katika mambo ya kidunia na kupuuza maisha ya kiroho, ingawa maisha ya kidunia yanaunda upande katika maisha ya mwanadamu na maisha ya kiroho (Akhera) yanaunda upande mwingine wa maisha hayo, bali ni kiini chake, na upungufu kama huu wa kiroho hautoshelezwi kwa mambo ya kidunia.


Kiuhalisia ni kuwa kila kitu kinaweza kupata uwiano kama mwili na roho vitapewa haki sawa sawa kwa kadri na kiasi cha kila mojawapo; yaani uwiano na mafanikio yatapatikana ikiwa tutatekeleza haki ya Allah kwa namna inayoendana na utukufu wake (s.w.t), na tukatekeleza haki ya Qur’an ipasavyo, na tukaielekea na kuithamini dunia kwa mujibu wa thamani yake na Akhera kama inavyostahiki.


Allah (s.w.t) anasema katika kitabu chake kitukufu:
“Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia . . .” (Al-Qasas 28:77)


Ndiyo, ni lazima kutumia vizuri aliyotuneemesha Allah katika afya, utajiri na akili na tujiandae na akhera kwa hayo, na wakati huo huo tusisahau fungu letu la dunia, hiki ndio kipimo cha Qur’an tukufu, lau kama uwiano utapatikana baina ya dunia na akhera kwa mujibu wa msingi huu wa Qur’an tusingepatwa na kiasi hiki cha huzuni.


Kisha ninasema kuwa hali halisi inatulazimu wakati wa kujadili kuhusu suala la malezi katika familia, kutafiti tunayoweza kuafikiana juu ya misingi ya kimaadili, hasahasa katika zama hizi ambazo ladha za kidunia zinamzuia mtu kumkumbuka Allah (s.w.t).

Kustawi, Kuporomoka Kwa Jamii na Uhusiano wake na Kanuni za Kimaumbile

Kila umma unapitia nyakati za kustawi na za kuporomoka, na hustawi kwa maadili ambayo yanaupa hadhi umma huo na unaporomoka kwa sababu zinazoshusha thamani yake; kwa sababu kanuni za ulimwengu zinatenda kwa namna ya kulazimisha na kushurutisha. Kwa vile asili ni sehemu ya ulimwengu, Allah ameiumba kidhahiri kuwa ni yenye kufuata kanuni hizi za lazima, na hivyo ni lazima kuchunga kanuni za asili na kanuni za kimaumbile, tukitegemea kanuni hizi zitusamehe makosa yenu, kisha tukafanya upungufu katika baadhi ya nyadhifa zetu, zitatutupa na kutumaliza.


Ndiyo, hakuna maghfira (msamaha) kwa kanuni za kimaumbile ambazo ni kanuni za sheria ya kimaumbile, kwani katu hazisamehi, tukifanya vizuri katika kuchagua mwenendo kwa mujibu wa kanuni hizi, Allah atatunyanyua kwenye ngazi ya juu kuliko vilivyo juu, na tukifanya upungufu katika kuchunga sababu tutaporomoka kufikia chini kuliko vilivyo chini, kama hatuto poromoka itakuwa ni kwa ajili ya fadhila na matakwa ya Allah (s.w.t).


Na kama tutarudi kwa mara nyingine kwenye tatizo kuu basi tunapaswa kujibu maswali yafuatayo: Je, tumetosheka kuwa kuna vichochezi hatari na sababu za kimakusudi za kuharibika kwa maadili? Na je, tunaamini kweli kuwa kuna tatizo la kimaadili? Na je, tunayatazama maisha yetu ya sasa yasiyo na utulivu kuwa ni uharibifu wa kimaadili au matokeo ya hali ya kawaida?
Itaendelea…

You might also like
Leave A Reply

Your email address will not be published.