Muendelezo wa Makala iliyopita.
Maisha Kulingana na Kanuni na Mipango
Uamuzi Sahihi Unategemea Mipango
Ni muhimu kuweka kanuni ambazo tutazitumia kuendesha maisha yetu tokea mwanzo. Ndiyo, tunapaswa kusema katika nafsi zetu: “Inanipasa kuupangilia mwaka huu katika namna hii, na mwakani katika namna hii, na mwaka utakaofuata katika namna hii.”
Tukifanya hivi tutazoea kuona mbele yetu yale tunayoyajuwa katika mipango na miradi, na tutachukua uamuzi sahihi kwa wepesi, hatutoangukia kwenye sintofahamu. Lakini tusipojiwekea misingi, na mipango kuhusu mustakabali, basi tunapaswa kujiandaa kuteleza- kwa kushangazwa- kuanzia kesho na kupelekwa kusiko julikana, Tujengeni taswira kuwa kuna mambo mengi yasiyojulikana yamevamia maisha yenu ghafla, je, kwa wakati huo mtakaa na kupiga makelele? Au mtafanya kitu gani! Hivyo ni lazima kufanya maandalizi kabla ya kutokea yote haya.
Kila Mtu Amekuwa Mtazamaji Tu
Tuitazame sasa hali ya ulimwengu wa Kiislamu ambao idadi ya Waislamu inafika bilioni moja na nusu, hapo tutaona kuwa watoto na wajukuu wanaungua katika tanuri moja walilochomwa wazazi, na katika moto huohuo ambao wao waliungua, wakati mmoja wao akiungua unamuona mwingine akiangalia bila ya kujali, na wakati ambao umma unazama katika kinamasi, tunawaona wengine wanaokuja baada yao wanafuata mwenendo wao bila ya kujuwa na kuingia katika dimbwi hilohilo chafu, na wanaonja huzuni chungu, na hawabaki katika kumbukumbu za watu ila kama kumbukumbu mbaya zinazochukiza.
Bila Mipango Tutajikuta Tunafuata Ya Waliyopita Hatua Kwa Hatua
Mtume (s.a.w) anasema akitoa habari na kuonya kama tulivyoeleza mwanzoni:
“Mtafuata mwenendo wa wale waliokuwa kabla yenu, shubiri kwa shubiri na hatua kwa hatua, hata kama wataingia katika shimo la kenge mtawafuata”.
Tunaweza kutohoa kutokana na hadithi hii onyo ambalo muhtasari wake ni kama ifuatavyo:
“Chukueni tahadhari, na zindukeni, na tembeeni kana kwamba mnatembea katika shamba lenye mabomu yaliyotegwa ardhini huenda ukatokea mlipuko muda wowote”.
Na hapa tutasimama katika beti za kishairi zenye kuhuzunisha ambazo amezitunga Mshairi wa Kiislamu Marehemu “Mehmet Akif” katika kujaribu kutoa picha ya Umma wa Kiislamu ulipo fikia.
Haya (aibu) imeanguka, Ubaya umeingia katika kila sehemu
Ni sura ngapi mbaya zilikuwa zikistiriwa na pazia/nikabu
Kuthamini wema kumetoweka, ulinzi wa ahadi umepotea, amana imebaki maneno tu!
Uongo umeenea, na hiana ipo kila sehemu, haki haijulikani.
Nyoyo zimekuwa ngumu, na matumaini yamekuwa chini, na hisia zimekuwa duni
Waja wa Allah wanadharaulika, Na viwiliwili vinatetemeka eeh Mola wetu,
ubaya uliyoje wa mageuzi haya!
Hakuna tena dini wala imani, dini imeharibika na imani imekuwa udongo
Fahari imepotea na dhamira zimenyamaza
Hakuna tena uhuru kwa kutoweka kwa maadili.
Ndio! Fujo na mmomonyoko wa maadili havijasambaa kwenye sehemu moja tu, bali sehemu zote, kiasi kwamba wale waliokuwa wakikereka na hali hii wamekuwa– kwa kuathirika na miale ya kukosa hisia- hawana habari ya kinachoendelea.
Maadili yenye Hadhi ya Juu
Mtume (s.a.w) anasema:
“Hakika nimetumwa ili kukamilisha maadili mema”.
Hakika neema za Allah kwetu hazihesabiki, na tumepewa vipawa na uwezo vinavyotuwezesha kuchukua nafasi yetu ya juu Zaidi baina ya wakazi ulimwengu (Al-Mala al- A’la) na kuthamini neema za kiungu alizotutunuku Mola wetu (s.w.t) ni katika kumtukuza Allah (s.w.t), na kuheshimu dhati yetu iliyopewa uwezo mwingi.
Hakika vitabu vya Allah (s.w.t) ni mwangwi wa ujumbe huu na pumzi yake, na mitume ndio wawakilishi wa kweli zaidi wa hakika hii, ama kipande cha mwisho cha mnyororo huu wa dhahabu ni Mtume Muhammad (s.a.w), na yeye ni dalili ya wazi zaidi ya hakika hii, na mfalme mkuu wa maadili ya juu. Allah (s.w.t) anasema katika surat Al-Qalam akiashiria ukubwa na upana wa maadili yake:
“Na hakika wewe una tabia tukufu”. (Al-Qalam 68:4)
Pambo la Maisha ya Dunia (Watoto na Mali)
Allah (s.w.t) anasema katika Surat Al-Kahf:
“Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini.” (Al-Kahf 18:46)
Aya hii Tukufu kiujumla inatilia mkazo kuwa Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia, na kuwa lina sehemu si ya kudharaulika.
Ndiyo, ni yenye kufuata sura mbaya ya kutoweka ya dunia, na sura hii inatazama dunia yenyewe, na ni sura yenye kuleta dhiki na kero. Na hii inaonesha kuwa mali kama mali si kitu cha kujifaharisha nacho, na mtoto pia si kitu cha kujifaharisha nacho, isipokuwa vikielekezwa kwa Allah na akhera vitafika kwenye thamani inayovuka vitu vyote vya thamani, na kuingia katika kundi la mazuri yenye kubakia, likitokea hilo vitakuwa huko akhera miti mikubwa inayojitangaza kwa matunda yake, ingawa vilikuwa mbegu duniani.
Mambo haya niliyojaribu kuyagusia ni misingi ambayo Qur’an Tukufu imetuwekea; inatuonesha njia sahihi zaidi na kutunuku uhai katika roho zetu, na ipo katika famasia ya Qur’an Tukufu na katika utaratibu aliyouweka Mtume (s.a.w) kwa mikono yake miwili iliyobarikiwa ambao ni Sunnah zake, na kuchukua uhai kutoka katika Qur’an Tukufu na Sunnah na kusikiliza mwangwi wa juu wa viwili hivyo, ni sehemu ya rehema mahsusi kutoka kwa Rahimu (s.w.t).
Tuwe na Huruma
Matokeo Ya Kukua Kwa Sayansi Na Tekinolojia
Qur’an Tukufu inaashiria ulazima wa watu kutaka msaada kutoka kwa huruma ya Allah pale wanapopatwa na tatizo lolote kama ilivyokuja katika kisa cha Nabii Ayyub (a.s):
“Na Ayyubu, alipomuita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.” (Al-Anbiya 21:83)
Ndiyo, kutaka msaada kutoka kwenye huruma ya Allah na rehema yake ni katika nafasi ya kuomba msaada kwake kwa ajili ya nafsi zetu, familia zetu, na watoto wetu– tuliyowaachilia mitaani– na jamaa zetu, na kutangaza pia udhaifu wetu na kushindwa kwetu, na kukiri na kusalimu amri kuwa Yeye (s.w.t) anashikilia hatamu ya kila kitu, ukiongezea kuwa huruma ni njia ya kuleta rehema, wenye kuhurumia watahurumiwa na Allah (s.w.t), tukiwa na utambuzi na wepesi kuhisi kuharibika kwa maadili Allah (s.w.t) atatulinda na kila uharibifu unaoweza kutokea kwetu.
Mtume (s.a.w) anasema:
“Wenye kuhurumia watahurumiwa na Rahmani, wahurumieni waliopo ardhini mtahurumiwa na aliye mbinguni”
Msiba Wa Kweli
Mauti ya kweli si mauti ambayo tunayajuwa na wala msiba mkubwa si mabalaa yanayoweza kutokea kama vile ajali za barabarani na mengineyo, bali umauti na msiba wa kiukweli kweli ni mtu kuisahau na kughafilika na nafsi yake, na kutokuwa na hisia, na kufa kwake katika ulimwengu wa moyo na kiroho.
Ndiyo, balaa kubwa ni mtu kutoweza kujuwa kuwa nyumba yake inaungua, na kubakia bila ya kuhisi uharibifu na uozo unaomsibu mwanawe. Ikiwa wazazi hawajui moto ulio ndani ya nyumba yao, huzuni iliyoje hiyo, na kughafilika kulikoje huko, na upotovu mkubwa kiasi gani huo, mfano wa wazazi kama hawa walie watakavyolia kwa ajili ya hali yao hii haitatosha, kwa sababu kulia nako kunahitaji moyo wenye hisia.
Itaendelea…
- Ibn Abdulbarr, At-Temhid 16/254, Al Bayhak, As-sunanul kubra 10/191
- Kwa mujibu wa Ustadh Said Nursi dunia ina nyuso tatu: uso wa kwanza unaelekea kwenye majina ya Allah na sifa zake. Uso wa pili unaelekea akhera kwa maana ya kwamba dunia ni shamba la akhera. Na uso watatu unaelekea kwenye matamanio ya nafsi na starehe na huu ndo uso mbaya ambao hautaki Allah (s.w.t). na huu ndio upande wa watu madhalimu ambao wanaamini kuwa hakuna maisha baada ya kifo.