
MALEZI YA WATOTO NA FAMILIA – 2
Muendelezo wa Makala iliyopita.
Kuiga Umma Nyingine
Mtume (s.a.w) anasema: “Mtafuata mwenendo wa wale waliokua kabla yenu, shubiri kwa shubiri na hatua kwa hatua, hata kama wataingia katika shimo la kenge mtawafuata”.
Sababu ya kuporomoka kwa jamii ambazo mmomonyoko wa kimaadili umetawala, inarejea kwenye kuhadaika na dunia, na kutoweza kufanikisha uwiano baina ya mwili na roho, na kushindwa kuyazuia matamanio ya nafsi; lakini kwa bahati mbaya tatizo hili lilianza kutokea mwanzoni mwa historia, tena likahama kutoka kizazi kwenda kwenye kizazi kingine kwa miaka mingi.
Halafu watu wa nchi za magharibi wakarithi mabaya haya, wakayapamba kwa ndoto za ustaarabu, wakahamisha kwa waigaji wao. Hivyo hadithi hii tukufu inazingatiwa kuwa muujiza wa kubainisha. Ndiyo, Mtume (s.a.w) alifunuliwa maana hii kwa ufunuo usio wa kusoma, kisha akauweka katika muundo wa maneno.
Kwa Nje Wanaonesha Ufahari Ndani Wanahuzuni
Hapa siwezi kuhamia suala jingine bila ya kugusia nukta ifuatayo: tunapoangalia katika baadhi ya mataifa na watu wake tutaona kuwa ni wenye kuishi kifahari na furaha kwa uwezo wao wa kimada(uwezo wa kumiliki vitu), na tunadhani kuwa wamemaliza matatizo yao yote, ingawa mtu wa magharibi daima anaishi katika hali ya huzuni na kuchanganyikiwa. Anaitaka furaha lakini haipati, na kiwango cha kujiua huko magharibi ni kikubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine.
Hatuwezi kujenga taswira ya umma unaoishi kwa furaha hali ya kuwa kiwango cha kujiua kinaongezeka baina ya watu wake waume kwa wake. Katika mkutano uliofanyika Rabat mji mkuu wa Moroco chini ya anuani ya “Kujenga familia” imeelezwa wazi kuwa kiwango cha talaka nchini Marekani kinafikia asilimia 40, na pengine kwa sasa idadi hiyo itakuwa imezidi. Hii ndio Marekani ambayo wengi wanaiona kuwa ni nchi inayoongoza kwa uwiano baina ya umma zilizomomonyoka kimaadili, huenda ikawa haijaathiriwa na uchafu wa magharibi kutokana na umakini wake katika baadhi ya masuala, na pamoja na hayo kuna tatizo la maadili huko pia.
Kiumbe aliyetukuzwa
Hapana budi kila kitu kuelekezwa na kufanywa kwa ajili ya furaha ya mwanadamu. Mwanadamu ndiye khalifa wa Allah katika ardhi yake, Allah amemuwepeshia ulimwengu; basi ni lazima kwa ustaarabu kuinuka kwa ajili yake na kutafuta furaha yake. Yeye ndiye kiumbe aliyekirimiwa zaidi; Allah anasema katika kitabu chake kitukufu:

“Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tukawabeba nchi kavu na baharini (tukawapa usafiri wa baharini na nchi kavu), na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba”. (Al-Isra 17:70)
Harakati Zote Zinalenga Furaha Ya Mwanadamu
Sheikh Ghalib anatilia mkazo ukweli huu kwa kusema:
“Itazame vizuri nafsi yako, wewe ni muhtasari wa ulimwengu
Na kiburudisho cha macho cha ulimwengu, huyu ndiyo wewe.”
Ndiyo, mwanadamu ni kiumbe aliyekirimiwa mbele ya Allah (s.w.t) na staarabu zote na harakati zote za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni juu ya ardhi havikuwa ila ni viashirio vya kukiri thamani yake, hakuna thamani ya harakati zozote ikiwa hazilengi furaha ya mwanadamu, au kuahidi uanadamu chochote.
Utawa na Kutawala kwa Kanisa Nchi za Magharibi
Matokeo Ya Kukua Kwa Sayansi Na Tekinolojia
Kuna tofauti kubwa kati ya ulimwengu wa Kiislamu na ulimwengu wa kimagharibi katika maudhui haya, hakika umeanguka utawala wa kitawa na Kikristo huko magharibi kutokana na uvumbuzi wa kisayansi kuwa juu. Ama hali katika ulimwengu wa Kiislamu ipo tofauti, ambapo kuelekea katika dini kumeongezeka sanjari na maendeleo ya kisayansi.
Kabla ya harakati za uamsho na matengenezo Ulaya, kiliwekwa kiwango kikubwa sana cha kodi kwa watu waliyo chini ya utawala wa kanisa, hadi watu wote wakapata hofu juu ya mustakabali wao kutokana na kanuni za kanisa zenye kubadilika mara kwa mara.
Viongozi wa kiroho walikuwa wakificha uadui mkubwa waliokuwa nao dhidi sayansi, wala hawakukaribisha kabisa vumbuzi za kielimu ambazo nyingi kati yake ziliishia kukataliwa bila ya kutazama hakika yake; na hawakuwa wachache waliyohukumiwa na mahakama za upelelezi kufanya kazi ngumu za kudumu kutokana na mambo tofauti waliyoyavumbua!
Watu hawakuwa na uwezo wa kupinga uelewa huu wenye kukandamiza, bali wengi wao hawakuweza- ukiwatoa wachache katika Waaristokrati (Aristocrats)– kuzungumza kuhusu kukandamizwa kwa mafakiri na haki za mwanamke ambaye walimzingatia kuwa ni nusu mtu, halipwi isipokuwa nusu, na kwa hivyo, ikasababisha sehemu kubwa ya jamii kukataa dini. Na kutokana na ukataaji huu wa pamoja, kila kilichohusiana na kanisa kikaanguka. Ni punde tu pale harakati za mageuzi zilipoanza katika sehemu tofauti; na hayo yakafuatiwa na mmomonyoko wa moja kwa moja wa maadili.
Uhusiano kati ya Dini na Nchi kwenye Uislamu;
Katika ulimwengu wa Kiislamu hayakuvunjika matumaini ya msomi yeyote; dini haikuwahi kufanya ukandamizaji wa aina yoyote kwa dola au wananchi, nguvu daima ilikuwa pamoja na haki, na viongozi walikuwa kwa ajili ya kuwahudumia watu, kiasi kwamba watawala wa Kiislamu walikuwa wakisikiliza neno lolote linalosemwa katika njia ya haki, na walikuwa wakionesha utayari wao wa kukubali haki.
Makhalifa waongofu mfano Umar Ibn Kha ab (r.a) na Ali Ibn Abi Talib– Allah autukuze uso wake– walikuwa wakienda na Yahudi kuhukumiwa mbele ya kadhi, na kwa vile nguvu daima ilikuwa pamoja na haki hakukuwa na uwanja wa kufanya ubabe abadan kama ilivyotokea huko magharibi, na kwa hiyo haikutokea kwa mtu yoyote kukataa dini, maisha wanayoyafikiria wengine kwenye kitabu cha “Utopia” yamekuwa maisha halisi katika ulimwengu huu wa Kiislamu.
Misingi ya Kimaadili
Maswali Ya Kujiuliza Ili Kurudi Katika Misingi
Kipi tunachokiona kizuri na kipi tunachokiona kibaya? Tutafikiri vipi jinsi ya kuwalea watoto wetu? Na je, kuna mkakati au shabaha tuliyoiweka kwa ajili ya kufanya jambo hilo? Vipi tunafikiri katika kuwalea watoto wetu? Tunasema: “Mimi nataka mwanangu awe hivi”, je, tumefanya nini ili kufikia katika hilo? Tunalionaje suala la watoto kuzagaa huku na kule na kuja usiku wakiwa wamechelewa?
Je, tutawafungulia milango yetu na vifua vyetu pale watakapokuja saa yoyote ya usiku? Ni matendo yepi tunayoyakubali kutoka kwa watoto wetu na kwa kiasi gani? Na matendo yepi tunayaona ya kimaadili na yepi si ya kimaadili? Na matendo yepi mazuri na yepi mabaya kwao? Na kwa kiwango gani tutawaruhusu kufanya yale wayafanyayo? Na kanuni gani tunayoitegemea katika suala la kuingilia katika mavazi yao?
Je, tumeshafikiria sasa hivi tutakachokifanya tusiporidhia jambo katika mambo yao? Je tumepata ufumbuzi wa hili? Ni milango mingapi tumegonga, na wataalamu wangapi tumewaendea? Na kiasi gani cha machozi tumedondosha ili kupata ufumbuzi wa hili? Maudhui haya yanatuhusu kama yanavyowahusu jamaa zetu na majirani zetu na umma wetu wote. Je, ni kweli tumefanya jitihada ili kupata ufumbuzi wa mambo haya yote?
Tunajipanga Vipi Katika Kutatua Tatizo?
Tusipokuwa na mkakati au malengo katika maudhui haya hii inamaanisha kuwa sisi tumekuwa- kama alivyoeleza Mtume (s.a.w) katika Hadithi iliyotajwa hapo kabla– tunafuata mwenendo wa wale wa kabla yetu, shubiri kwa shubiri na hatua kwa hatua na hivyo kuingia katika jahanamu, ni mafikio mabaya yaliyoje?
Na uhalisia ni kuwa yote haya ni kutokana na kuwa kwetu mbali na Allah (s.w.t) na Mtume wake na Qur’an Tukufu na kufuata kwetu matamanio yetu. Wazazi wengi leo wanateseka kutokana na baadhi ya watoto wao, je, tumefikiria nini katika kutibu makosa yao? Tusipuuze umuhimu wa kufikiri katika jambo hili.
Ndiyo, lazima tufikirie kama hivi, na turudi kwenye nafsi zetu na kujiuliza swali hili: Nini kiukweli tunachoweza kufanya katika jambo kama hili? Je, sisi ni wenye kusamehe yote haya yanayoendelea au hatuna hisia au ni kwamba hatujali? Je, tutosheke kutazama yanayojiri katika nyumba zetu tukiwa kimya kama vile hatuna hisia? Au tutafute ufumbuzi wa kila dogo na kubwa ndani ya nyumba zetu?
Tunaweza kwenda katika muktadha huu na kujiuliza maswali mengine, mfano: Je, tumemfuatilia mtoto wetu tukiwa kama mlinzi mwaminifu? Na je, tumefanya jitihada za kuwajua marafiki zake? Na je, tumeweza kumtengenezea mazingira yanayomfaa daima? Na ni aina gani ya watu tuliyomtambulisha kwao mpaka sasa? Tusipofanya hilo atacheza na nani? Je inatosha kumuandikisha katika shule au kumkabidhi kwa mwalimu, au kumuandikisha katika kozi ya kuhifadhi kitabu cha Allah (s.w.t)? na je inatosha kumjulisha msikiti na kumkabidhi kwa imamu? Ukiacha umuhimu wa kutafuta majibu ya maswali haya yenye kuingiliana ni muhimu pia kuyafanya maisha yetu binafsi kuwa na utaratibu, kina, ikhlasi, uvumilivu na mvuto.
Itaendelea…